Na Hazard Mpango

Mwansaoka nguli duniani, Mbazil Edson Arantes do Nascimento maarufu Pele alipata kunukuliwa akisema kuwa mafanikio sio ajali bali ni utendajikazi wa nguvu, uvumilivu, kujifunza, na kujitoa mhanga.

Kubwa zaidi ya yote hayo, Pele aliyezaliwa Oktoba 23, 1940 na kuwika zaidi na timu yake ya taifa ya Brazili ‘Samba Boys’ miaka ya 1957 hadi 1971 alisisitiza kuwa ni kupenda unachofanya au unachojifunza.

Ujumbe wa Pele nauona kama vile haujabagua wa kuwafikishia. Ameutuma kwa walimwengu wote wanaotaka mafanikio kwenye nyanja yoyote maishani mwao pasi na kujali ni kisiasa, kijamii au kiuchumi.


Hata mashabiki wa soka nchini nao wameguswa. Salamu za gwiji huyo wa kandanda duniani ziwafikie na wao pia, lakini iwapo watakuwa wanataka mafanikio ya kweli kwenye mawanda ya soka.

Ni maneno ya hamasa kwao yanayowasukuma mashabiki wa soka letu la bongo kujisaili iwapo malengo yao yamefikia au la. Ni changamoto kubwa inayowapasa kutulia kuona namna bora ya kuitatua.

Mashabiki wenyewe wanajua na bila ya shaka wanajifunza kutoka kwa wenzao wa nje ya mipaka ya nchi yetu na hasa wa Uingereza. Wanawaona jinsi wenzao wanavyowachachafya makocha, wachezaji na wenye hisa kwenye timu.

Wanawaona wenzao namna wanavyopambana ili kusaidia mafanikio ya timu zao badala ya kulia, kupiga kelele tupu uwanjani na kujipaka majivu usoni. Wenzao huko wanajitoa mhanga wa kweli kiasi wanapozuiwa uwanjani timu inaathirika.

Kinyume na mashabiki wengi wa soka la bongo ambao wao wapo nyuma na soka lenyewe. Hawawazi mafanikio ya kweli zaidi ya kungoja ajali itakayowezesha soka la bongo lifanikiwe.



Hawataki kuumia kutokana na kupigania soka iwe ni kufa au kupona. Wenyewe wamechoka kifikra, hawaoni mbali kuhusu soka kwa ujumla ukiachana na mapenzi zaidi yaliyokolea ya timu kongwe za Simba na Yanga.

Hawaamini kuhusu ubingwa wa nje ya mipaka ya nchi kuanzia ngazi za vilabu na taifa. Miaka mingi vilabu vya nchi yetu vimekuwa wasindikizaji kwenye mashindano makubwa barani Afrika, lakini mashabiki hawajali.

Timu za taifa nazo zimekuwa ‘tia maji tia maji’ miaka kibao, lakini mashabiki wamekuwa kimya kama sio wao vile. Wanaacha soka likititia bila ya kelele ilhali nao wana nafasi ya kuliokoa.

Tatizo ni kuendekeza Simba na Yanga kwa kiasi kikubwa na kusahau kuhusu soka. Vizazi vinarithishana kushabikia zaidi timu hizi ambazo zimeishia kupokezana ubingwa wa ligi na mashindano ya nyumbani na yale ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Hebu tazama mfano timu kongwe ya Yanga ambayo imenzishwa tangu mwaka 1935 imeachwa nyuma na timu ya Asante Kotoko ya nchini Ghana iliyoanzishwa mwaka huohuo ambayo imechukua ubingwa wa Afrika mara mbili.

Imeshindwa na AS Vita Club ya Kinshasa pamoja na CARA Brazzaville ya Jamhuri ya Kongo ambazo zimeanzishwa mwaka mmoja na kupishana miezi, lakini timu hizo zimeshachukua ubingwa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mara moja moja.

Pia Simba S.C iliyoanzishwa mwaka 1936 imeshindwa kusafisha nyota kama walivyofanya wenzao State d’Abidjan ya nchini Ivory Coast ambayo imechukua ubingwa wa Afrika mara moja.

Ukiachana na timu zilizopata mafanikio ingawaje zimeanzishwa mwaka mmoja na klabu zenye mashabiki wengi nchini bado kuna timu nyingine zimeanzishwa miaka kadhaa baada ya timu zetu na bado zimenyakua ubingwa wa Afrika.

Mfano wa timu ya ES Setif ya Algeria imeanzishwa mwaka 1958 tayari imeshanyakua mara mbili, Enyimba F.C ya nchini Nigeria imeanzishwa mwaka 1976 nayo imechukua mara mbili ubingwa huo wa klabu barani Afrika.

Timu kamaWydad Casablanca ya Morocco ilianzishwa mwaka 1937, Orlando Pirates F.C ya Afika Kusini, Asec Mimosas ya nchini Ivory Coast zilianzishwa mwaka 1948, Union Douala ya nchini Cameroon na FAR Rabat ya Morocco ailianzishwa 1958, zote zimechukua mara moja moja wakati klabu ya Hafia F.C ya nchini Guinea iliyoanzishwa mwaka 1953 imechukua ubingwa wa Afrika mara tatu.

Hebu mashabiki wetu wa soka waache Usimba na Uyanga waangalie kuhusu soka kwa ujumla. Wasiishie kupiga kelele wajitoe mhanga kwa kadiri ya uwezo wao ili yapatikane mafanikio kwenye soka ingawa hatumlaumu dobi kutakasa kaniki.

27 Feb 2017

0 maoni:

Chapisha Maoni

:) :)) ;(( :-) =)) ;( ;-( :d :-d @-) :p :o :>) (o) [-( :-? (p) :-s (m) 8-) :-t :-b b-( :-# =p~ $-) (b) (f) x-) (k) (h) (c) cheer
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.

 
Top