Na Azard Mpango #UO 2
Kama vile ni mazingaombwe au uchawi kwa namna alivyokuwa akifanya vitu vyake uwanjani. Alichezea mpira atakavyo, aliwapindua wapinzani wake kwa kadiri alivyotaka na ilikuwa ni nadra mno mpira kupotea miguuni mwake. Aliwapa wakati mgumu waliotaka kupambana naye kipindi akiwa na mpira miguuni mwake kutokana na kuwa na chenga zenye maudhi zilizoacha uzito kwa mpinzani aliyekuja kumkabili.

Alisifika kwa mbinu na maarifa ya hali ya juu awapo uwanjani. Alitumainiwa kipindi chote kutokana na uhodari wa kubadili hali ya mambo mchezoni na zaidi hakuwa mchoyo wa kutoa pasi. Mahali ambapo hakuna anayetarajia kupita bado jamaa huyu aliweza na pengine hata kufunga. Baadhi ya magoli yake amefunga akiwa chini ya ulinzi mkali wa wapinzani kiasi cha kuwaduwaza wengi.

Ni kweli kuwa kila zama zina yake lakini tangu zama zake nahata zinazoendelea bado anasakwa atakayelingana naye. Aliitwa ‘Mchawi wa Mpira wa Miguu’ na akanadiwa kuwa ni mchezaji bora zaidi wa Nigeria ambaye hajapatapo kutokea katika zama zake. Hakuwa na wa kumshindanisha kwa kipindi hicho na baadhi ya wataalamu wa soka wanaamini hivyo mpaka sasa bado hajatokea Muafrika wa aina yake.

Huyu ni Augustine Azuka Okocha aliyezaliwa Agosti 14, 1973 maeneo ya Enugu nchini Nigeria. Alikuwa akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na alipendelea mno kuvaa jezi namba 10 mgongoni. Kama wachezaji wengine hasa kutoka bara la Afrika ambao historia zao za soka zinaanzia kwenye vilabu vya mitaani, naye Okocha alianzia huko na kisha klabu ya Enugu Rangers iliyomtoa golikipa maarufu nchini Nigeria, William Okpara.

Alizoeleka kwa jina la ‘Jay-Jay’ Okocha ambalo chimbuko lake ni James Okocha kaka yake aliyeanza kucheza mpira wa miguu kabla ya Augustine (mdogo mtu). James ndiye aliyekuwa amepewa jina la mitaani ‘Jay-Jay’ lililokuja kuhamia kwa mdogo wake kiasi cha mwenye jina hilo kufunikwa na pengine mpaka leo baadhi kutotambua asili ya jina hili.

Maisha matamu ya soka ya Okocha yalianzia nchini Ujerumani alipokwenda kumtembela rafiki yake mmoja miaka ya 1990, ambaye alimshauri kufanya majaribio katika klabu ya Borussia Neunkirchen iliyokuwa daraja la tatu wakati huo na alifanikiwa kupata nafasi kutokana na soka safi alilokuwa akilitandaza uwanjani.

Akiwa nchini Ujerumani mwaka 1992 alijiunga na klabu ya Eintracht Frankfurt ambapo alikutana na mchezaji maarufu mwafrika kutoka nchini Ghana, mshambuliajiu Tony Yeboah na baadaye akajumuika na mshambuliaji maarufu Thomas Doll raia wa Ujerumani. Mwaka 1993 goli zuri alilomfunga mlinda mlango Oliver Kahn lilichaguliwa na watazamaji wa kipindi cha michezo cha ‘ARD German TV sports program’ kuwa goli la mwaka.

Mwaka 1995 Okocha alihama Eintracht Frankfurt na akabadili upepo wa Ujerumani kwa kuelekea nchini Uturuki akajiunga na klabu ya Fenerbahce. Katika msimu wake wa pili kwenye klabu yake nchini Uturuki, Okocha alifunga magoli matatu ya ajabu ambayo hayataweza kusahaulika ndani ya klabu yake. Akiwa nchini Uturuki humohumo Okocha alichukua uraia wa nchi hiyo na kutumia jina la Muhammet Yavuz.


Maisha ya soka ya ‘Jay-Jay’ Okocha, mwaka 1998 yalihamia nchini Ufaransa ambapo alijiunga na klabu ya Paris St-Germain (PSG) mahali alipokutana na Mbazil Ronaldinho Gaucho. Hata hivyo katika majira ya joto mwaka 2002 baada ya Kombe la Dunia alijiunga na klabu ya Bolton Wanderers ya nchini Uingereza.

 Mashabiki wa Bolton walimpokea vyema na kumkubali huku msimu wake uliofuata alipewa unahodha 
ambapo aliiongoza klabu yake mwaka 2004 katika Kombe la Ligi ambalo timu yake haikuwahiu kushiriki takribani miaka tisa.

Hata hivyo mwishoni mwa msimu wake klabuni Bolton alikwenda Qatar kujiunga na klabu ya  Qatar SC ambapo baada ya msimu mmoja tu nchini Qatar, mwaka 2007 alirejea Uingereza na kujiunga bure na klabu ya Hull City. Na kwa upande wa timu ya taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles, Okocha alianza kuonekana mwaka 1993 mpaka 2006.

Ajabu yake ni kwamba tangu aanze kucheza soka hakuwahi kushinda tuzo ya mwanasoka bora Afrika hata mara moja kama walivyoshinda akina Samuel Eto’o, Yaya Toure na wengine. Lakini bado Okocha aliwaambia mashabiki wake kuwa analishukuru Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) ambao ndio waandaaji na watoaji wa tuzo hizo akisema kuwa ameweza kutambulika na kupata tuzo nyingine.


Jambo kubwa na la msingi ni kwamba Okocha abakie kuwa darasa kwa wachezaji wetu. Badala ya kuishia kusoma historia yake wajifunze na vitu vyake alivyokuwa akifanya uwanjani. Okocha sio malaika aliyeshushwa toka mbinguni hivyo basi hata wachezaji wetu wanaweza japo sio kufikia balaa zake zilizompelekea kuitwa ‘Magic of Football’ lakini wakachota sehemu ya ufundi wake kama alivyochota Ronaldinho Gaucho. Watanzania nao wajifunze kwake.
06 Apr 2015

0 maoni:

Chapisha Maoni

 
Top