Na Azard Mpango

Siku za hivi karibuni kumeripotiwa kupatikana kwa mkanda wa video unamuonesha mtu aliyevalia mavazi meusi (kama ninja) na miwani ya giza aliyejiambulisha kuwa anaitwa Kais bin Abdullah, na kuthibitisha kushiriki katika uvamizi wa baadhi ya vituo vya polisi, kupora silaha, kuua na kujeruhi askari polisi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ni kwamba bin Abdullah alidai kushiriki kufanya vitendo hivyo viovu na vya kikatili kwa ajili ya kulipa kisasi cha siku nyingi. Anadai kuwa wenzao saba kutoka mkoa Mtwara wamekamatwa kwa makosa ya dhulma, kupanga na ugaidi.

Anawataja wenzake wengine 21 kwamba wamekamatwa huko Zanzibar na wamepelekwa gereza la Segerea jijini Dar-es-Salaam, 18 kutoka Mwanza wamepelekwa gereza la Kisongo, Arusha na wengine 19 wameuawa kabisa huko mkoani Mtwara.

Bin Abdullah anadai kuwa subira yao imefika kikomo na walichokuwa wakisubiri Mungu ameshawapa na badala yake kupitia video hiyo inayoonekana kulisakama jeshi la polisi nchini wametoa ahadi kwa kusema:"...kilichopo hivi sasa tunatoboa jahazi wote tuzame."

Ahadi hiyo na nyingine zilizokuwemo ndani ya video hiyo ni taa nyekundu ya tahadhari kwa jeshi la polisi, serikali pamoja na vyombo vyake vya usalama kuwa makini na utayari kwa lolote lile.

IGP Mangu akisisitizajambo

Lisipuuze na kuyaona ni mambo ya kisiasa au ni uongo na uzushi mkubwa na badala yake liamke na kuanza kufuatilia. Lijipange kwa mapambano, lijilinde na kuwalinda wananchi ambao hawana hata elimu au mbinu yoyote ya kukwepana na mashambulizi kama haya na pengine hawajawahi kukutana nayo.

Kujihadhari kabla ya hatari ni vyema kuliko kuingoja. Raia wanaliangalia jeshi la polisi ambalo bin Abdullah ameliandama huku akikumbushia uvamizi wa baadhi ya vituo vya polisi, kupora silaha, kuua na kujeruhi askari polisi.

Niseme tu kwamba hata kama video ya bin Abdullah ni ya vitisho au ina malengo mengine, bado jeshi hilo lisipuuze na kujiona lipo salama au hakuna atakayeweza kuwadhuru raia ambao jeshi la polisi lina dhamana ya kuwahakikishia usalama wao pamoja na mali zao.


Madhila dhini ya jeshi la polisi yalikuwepo na bado yanaendelea hivyo jambo la msingi ni kujipanga kwa jeshi hilo. Mathalani ni mara nyingi vituo vya polisi vinavamiwa na wananchi wanaoitwa wenye hasira kali na kuvishambulia vituo hivyo na hata pengine kuleta uharibu katika vituo hivyo.

Pia siku za hivi karibuni, jeshi letu la polisi limezidi kuandamwa. Ukiacha kuvamiwa kwa askari wake kipindi wakiwa kwenye maeneo yao ya kazi akama ilivyowatokea askari wenye namba G369PC Mansour na HV507PC Mwalimu, wakiwa doria ya pikipiki walinyang'anywa silaha zenye namba 14301230 na 143035 bado vituo vyao navyo vinavamiwa na kufanyika uporaji na pengine mauaji.

Mfano, Juni 2014, moja ya kituo kidogo cha polisi huko mkoani Pwani kilivamiwa na watu wenye silaha za jadi, walimjeruhi vibaya askari mwenye namba D9889 Koplo Joseph Ngonyani aliyekufa wakati akitibiwa hospitali ya wilaya, Mkuranga na askari Mariamu Mkamba alijeruhiwa (amepona baada ya matibabu), lakini wavamizi walipora silaha.

Septemba 2014, kituo kikubwa cha polisi cha Ushirombo kilichopo wilaya Bukombe, mkoa Geita kilivamiwa na katika uvamizi huo wameuawa askari polisi wenye namba WP7106Pc Uria Mwandiga na G2615PC Dustan Kimati, wakati askari polisi wenye namba E5831CPL David Ngupama na H627PC Mohamed Hassan walijeruhiwa na wavamizi walipora silaha.

Januari 2015, kituo cha polisi Ikwiriri, wilaya Rufiji mkoani Pwani kilivamiwa na kuuawa askari polisi wawili wenye namba E8732 Koplo Edga Mlinga (askari wa kikosi cha usalama barabarani) na WP5558 Judith Timoth na wavamizi walipora silaha wakati mapema mwezi Februari mwaka huu, kituo cha polisi Mngeta, wilaya Kilombero mkoani Morogoro kilivamiwa na kuibiwa baadhi ya vitu ikiwemo silaha yenye risasi zaidi ya 20, kutoka na msako wa polisi vitu hivyo vilipatikana na baadhi ya watuhumiwa wamekamatwa.

Kwa matukio haya na mengine yanayoliandama jeshi letu la polisi, bila shaka ni kengele ya kuamsha umakini wa jeshi hilo kuanzia kwenye vituo vyao ambavyo 'bin Abdullah' anajisifu kuwa wameweza kuchukua silaha hali wenyewe (wavamizi) hawakuwa na silaha. Umakini huo pia unapaswa uwe kwa nchi nzima kutoka na ukweli kuwa macho ya wananchi yanawatazama.

Video ya 'bin Abdallah' ilisahaulishe jeshi ile hadithi yao ya visu vya Chama cha Wananchi-CUF na nyingine zinazonasibishwa kisiasa zaidi. Jeshi la polisi liamke na kufuatilia kwa umakini wa hali ya juu uhalifu unaotamalaki kiasi inafikia raia kulinyooshea kidole jeshi hilo kuwa limeshindwa si tu kuwalinda wananchi bali hata kujilinda.

Wananchi nao wasikubali kuunga mkono aina yoyote ya uhalifu na kinyume chake washirikiane bega kwa bega na jeshi la polisi ili kutokomeza vikundi vinavyoweza kuingiza nchi yetu katika mabalaa kama yale ya Al-Shabab ya Somalia na Boko Haram ya huko Nigeria.

Jeshi la polisi nalo liumize kichwa usiku na mchana ili kupata mbinu ya kuwanasa wavamizi wa vituo vyao na ikiwezekana kurejesha mikononi mwao silaha zilizoporwa au kuibwa kwa sababu zitatumika kufanyia uhalifu mwingine ikiwemo kulipia kisasi cha siku nyingi kama alivyosema 'bin Abdullah' kwenye mkanda wa video ulioripotiwa kuwepo hasa Dar-es-Salaam.


Tunakiri kuwa tumepata hasara isiyolipika kwa kuwapoteza ndugu, jamaa, rafiki na wasimamizi wetu pamoja na mali zetu, hivyo naliomba jeshi la polisi lisipuuze kipenga cha hatari ya ugaidi kilichopulizwa na Kaisi bin Abdullah.
14 Feb 2015

1 maoni:

  1. ni kweli jeshi letu linapaswa kuwa makini kwa suala hilo pia sisi wananchi tushirikiane na vyombo vyetu vya usalama hili ni tatizo

    JibuFuta

:) :)) ;(( :-) =)) ;( ;-( :d :-d @-) :p :o :>) (o) [-( :-? (p) :-s (m) 8-) :-t :-b b-( :-# =p~ $-) (b) (f) x-) (k) (h) (c) cheer
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.

 
Top