Karibu nchi zote barani Afrika zinatumia katiba kama
muongozo na sheria mama. Katiba ndicho kitabu kitakatifu katika nchi ambacho
hufuatwa na raia wote na kuheshimiwa. Kutii katiba ni lazima si tu kwa
watawaliwa bali hata kwa watawala wa ngazi za chini na juu.
Ni mwiko kuifanyia kitendo chochote cha kuonesha
kuidharau katiba ya nchi na kufanya hivyo ni kosa ambalo huenda likapelekea
kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Pia kuvunja katiba ni kwenda kinyume na
sheria kwa yeyote yule awaye.
Mfano nchini Tanzania aliyekuwa mwasisi na
Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) daktari wa mifugo Leo
Lwekamwa aliwahi kuikanyaga katiba ya nchi mwishoni mwa mwaka 1997 katika
viwanja vya Jangwani.
Nyendo za baadhi ya viongozi wa juu katika nchi za
Afrika kama vile zinaanza kutisha. Hatua nzito wanazopiga huku wakiangalia
pembeni zinatoa ishara mbaya ya kutaka kuonesha dharau ya kukanyaga katiba
ambazo wenyewe ndio wasimamizi wakuu.
Polepole wanakaribia kuzisigina lakini kwa sauti ya
ukali kabisa wenyewe wanadai wanafanya marekebisho, ambapo ajabu yenyewe
marekebesho yanataka kufanyika wakati wakiona viatu walivyovaa wanapaswa kuvua.
Haviwatoshi wamekua.
Kama vile hawasikii sauti za waliokuwa pembeni
wakiwatazama na kuwakumbusha kuwa hatua wanazopiga ni kukimbilia kukanyaga
kitabu kitakatifu kinachofuatwa na watu wa dini mchanganyiko, hadhi na rangi
tofauti.
Wanataka kukanyaga makusudi kwa sababu vilivyomo
ndani yake havina urafiki nao. Badala ya kukaribishwa wanaagwa hali
wameshanogewa au hofu ya kuwa peku baada ya kutembea kwa muda mrefu tena kwa
kishindo kikubwa ardhini huku wametinga viatu vya bei mbaya.
Maneno mfano wa haya yaliyokuwemo katika Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, toleo lake la 2005 ibara ya 40
(2) yasemayo: “Hakuna mtu atakayechaguliwa zaidi ya mara mbili kushika kiti cha
Rais.” Hawayapendi na ndio hayo yanapelekea kunadi marekebisho mapema.
Rais wa Rwanda na kiongozi wa chama cha Rwandan Patriotic
Front (RPF), Paul Kagame aliyezaliwa Oktoba 23, 1957 huko Tambwe, Ruanda-Urundi
(Nyarutovo ya sasa), anatarajiwa kumaliza muhula wake wa pili mwaka 2017 na
katiba ya Rwanda haimpi ruhusa ya kuongoza kwa muhula mwingine.
Wakati Rais Kagame akiwa kimya, vyama vitatu vya
upinzani kikiwemo PDI cha Waziri wa Mambo ya Ndani, Musa Fazil Hererimana, PSP
na tawi la chama cha PS-Imbarakuri vimeonesha kumhitaji Rais Kagame aendelee
kuongoza.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Joseph Kabila aliyeingia madarakani baada ya
kuuawa na wanajeshi baba yake Laurent Desiree Kabila mwaka 2001, amekusudia
kufanya mabadiliko kipengele namba 220 cha katiba ili ikiwezekana aweze
kushiriki uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2016.
Kabila aliyezaliwa Juni 4, 1971 katika mji wa Hewa
Bora mkoa Kivu na alipata kusoma katika mikoa ya Dar-es-Slaam na Mbeya huku
akisemekana kutumia jina la Hippolyte Kanambe Kazemberembe Kabange Mtwale kwa
sababu za kiusalama anamalizia muhula wake wa pili na tayari baadhi ya wapinzani
wameshaanza kupinga harakati hizo. Katiba yao ni mihula miwili.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe
Msemaji wa Ikulu ya Bujumbura, Willy Nyamitwe
amethibisha kuwa Rais Pierre Nkurunziza aliyezaliwa Disemba 18, 1963 anatarajia
kugombea kwa muhula wa tatu iwapo chama chake ambacho yeye ndiye Mwenyekiti cha
National Council for the Defense of Democracy Forces for the Defense of
Democracy (CNDD-FDD) kitamchagua.
Huko Oagadougou, Burkinafaso sauti za wananchi
wanaozuia wakubwa wasikanyage katiba kwa ajili ya kuendelea kuishi Ikulu,
zimemuondoa kabisa mwaka 2014 Rais wa tangu mwaka 1987, Kapteni Braise
Compaore’ aliyezaliwa Februari 3, 1951 ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha
Congress for Democracy an Progress (CDP) na yuko uhamishoni nchini Morocco.
Rais
Abdoulaye Wade wa Senegal aliyepewa ruhusa ya kuongoza mihula mitatu na
Mahakama ya Katiba huku wananchi wakipinga kitendo hicho cha Rais kuwa
kimevunja katiba, alikubali kushindwa na mpinzani wake Macky Sall. Wananchi
walimkataa kwa wingi Wade aliyekanyaga katiba.
Mzee ‘Jongwe’ wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe
aliyezaliwa 21 Februari 1924 aliyeingia Ikulu
tangu 1987 bado yuko madarakani kwa zaidi ya miaka 20 na katiba
iliyopitishwa miaka ya usoni imeweka ukomo wa miaka mitano kwa muhula mmoja.
Rais wa Guinea ya Ikweta ambaye ni mwanajeshi wa
zamani Teodoro Obiang Nguema aliyezaliwa Juni 6, 1942 maeneo ya Acoacan,
Spanish Guinea aliyempindua mjomba wake Fransico Macias Nguema, mwaka 1979
hajaonesha nia kama anahitaji kugombea tena urais na inasemakana mwanaye
anatazamiwa kurithi iwapo Rais huyo ataachia madaraka hayo.
Rais Yoweri Kaguta Museveni aliyezaliwa Agosti
15,1944 maeneo ya Ntungamo, Uganda amekuwa Rais wa Uganda tangu 1986. Museven
aliyewahi kusoma Chuo Kikuu cha Dare-es-Salaam na kiongozi wa chama cha
National Resistance Movement (NRM) aliitisha uchaguzi wa vyama vingi wa kwanza
mwaka 2006 na aliushinda upinzani.
Itoshe kusema kwamba katiba zilizotungwa na
wawakilishi wa wananchi ziheshimiwe ili kulinda machafuko yanayopelekea
kupoteza roho za makumi kwa mamia ya wananchi. Inatosha yaliyotokea Libya,
Misri na Tunisia kuwa funzo kwa viongozi wakuu wa nchi za Afrika kuheshimu
katiba na kuachia madaraka pale inapobidi.
0 maoni:
Chapisha Maoni