Na Azard Mpango
Siku ya hafla fupi ya
kuagwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanzania na wa pili kwa Tanganyika
mzee Rashid Mfaume Kawawa (maarufu Simba wa Vita) alipokuwa anastaafu rasmi
siasa za majukwaani aliahidi kufa akiwa mwanachama muaminifu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Kawawa miongoni mwa
waasisi wa CCM alizaliwa Februari 26, 1926 katika kijiji cha Matepwende, wilaya
Songea mkoani Ruvuma alikufa mwezi Disemba mwaka 2009, aliyasema hayo mbele ya
swahiba wake Mwalimu Julias Kambarage Nyerere.
Mwalimu Nyerere ambaye
ndiye Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, chama kilichotokana na muungano wa vyama
viwili ambavyo ni Tanganyika National Union (TANU) cha Tanganyika na Afro
Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar, alipopata nafasi katika hafla hiyo alimjibu
Kawawa.
Nyerere aliyezaliwa
tarehe 13 mwezi Aprili katika kijiji cha Butiama mkoani Mara, ambaye kitaaluma
ni mwalimu alikufa tarehe 14, Oktoba 1999 huko London, Uingereza katika
hospitali ya Mtakatifu Thomas alikopelekwa akisumbuliwa na kansa ya damu.
Mwalimu Kambarage Nyerere
Aliongoza Tanganyika kama Waziri Kiongozi
katika utawa wa kikoloni (1960-1961), Waziri Mkuu wa Tanganyika (1961-1964),
Rais wa Tanganyika (1962-1964) na baadaye Rais wa Tanzania mpaka alipoamua
kuachia madaraka kwa hiyari Novemba 5, 1985.
Mwalimu Nyerere
aliyesimamia kuungana kwa TANU alichokuwa akikiongoza na ASP kilichokuwa chini
ya hayati Sheikh Abeid Amani Karume, katika hafla hiyo alimwambia Kawawa kwamba
ana roho ngumu kwa kuahidi kuifia CCM.
“ Rashid una roho
ngumu, utakufa mwanachama muaminifu wa CCM? Mimi siwezi kuyasema hayo, CCM
inaweza kubadilika. Siku ikiacha misingi nami naachana nayo, kwa sababu si mama
yangu,” aliyasema Mwalimu mbele ya mzee Kawawa aliyeahidi kufa katika uaminifu
na CCM.
Leo Simba wa Vita
aliyeahidi kuifia CCM hayupo, Mwalimu aliyeikana CCM kama ikiacha misingi yake
naye pia hayupo lakini matukio pamoja na nukuu zao zitabaki kama vielelezo kwa
wafuasi wa vyama vya siasa hasa CCM ili waweze kujifunza.
Wajiulize ni kwanini
muasisi na Mwenyekiti wa kwanza wa chama kikongwe nchini aliwahi kukikana chama
chake? Wafuatilie kwa kina hiyo misingi yenyewe ya CCM kwamba bado inafuatwa
ili hata kama Mwalimu Nyerere angekuwa hai aendelee kuwa mwana-CCM.
Hakuna tatizo kwa
Rashid kwa sababu aliahidi kufa ndani ya CCM hata kama kikipoteza dira lakini
alama ya kiulizo ibaki kwa Mwalimu ambaye ni mfuasi mtiifu wa itikadi ya
Kijamaa na Kujitegemea kuwa angeendelea kuwa mwana-CCM mpaka sasa? CCM hii bado
inalinda misingi yake kweli?.
Moja ya misingi ya CCM
ni kwamba Ujamaa na Kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu
waliosawa na huru. Hata Mwalimu Nyerere analisisitiza hili la usawa kwenye
chapisho lake la Ujamaa la mwaka 1962. Je msingi huu bado upo CCM hii
inayoadhimisha kuzaliwa kwake kila ifikapo Februari 5?.
Tarehe 5, Februari 1967
Mwalimu alianzisha Azimio la Arusha ikiwa ni msisitizo wa vitendo katika
kutekeleza itikadi ya Ujamaa lakini mwaka 1992, Halmashauri Kuu ya CCM
ilipitisha azimio la Zanzibar ambalo lilionekana kufungua milango ya utegemezi
kwa kukubali matakwa ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa.
Kupitia azimio hilo CCM
ilikubali sera ya vyama vingi, ilipokea ubinafsishaji uliokaribisha wawekezaji
na kuruhusu soko huria na utegemezi. Azimio la Zanzibar kama vile liliua rasmi
lile la Arusha ambalo lilizaliwa tarehe na mwezi unaofanana na wa CCM lakini
limefifilizwa.
Tunakumbushwa kuwa miongoni mwa misingi ya CCM
ni kwamba binadamu wote ni sawa. CCM hii inakiri hilo? Leo tunauzungumzia usawa
upi wakati kuna masafa marefu baina ya watawala na watawaliwa, masikini na
matajiri? Mwana-CCM yupi anakumbuka kutekeleza msingi huu wa usawa?.
Misingi ya CCM ilianza
kupindishwa tangu uhai wa muasisi wake na inaelekea kufukiwa kiasi cha
kuwafanya baadhi ya makada waanze kukitofautisha chama hicho, mfano aliyewahi
kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa nchi mzee Joseph Sinde
Warioba alisema yeye ni mwanachama hai wa CCM lakini sio CCM ‘maslahi’. Mwalimu
aliikana CCM ipi sasa?
0 maoni:
Chapisha Maoni