Na Azard Mpango #UO 2                           

Siku za hivi karibuni katika mkoa wa Tanga kumezuka taharuki kiasi cha kutikisa hali ya amani na utulivu nchini. Vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na baadhi ya watu wamekuwa wakitoa taarifa wanazozijua kuhusiana na tukio hilo..

Wapo waliodai kwamba kilichokuwa kikiendelea huko Tanga ni mapambano baina ya jeshi la polisi lililoomba msaada Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) na magaidi tena wakiwataja kuwa ni Al Shabbab toka Somalia.

Kuna waliokuwa wakitoa idadi isiyothibitishwa ya majeruhi na vifo na wengine hasa kwenye mitandao ya kijamii wakijaribu kuweka picha ambazo si za tukio halisi kiasi cha kuwapa hofu wananchi zaidi wasiokuwepo eneo la tukio.

Baadhi ya waliopata fursa ya kutumia kalamu walihamisha tukio hilo ambalo lilitawaliwa na piga nikupige ya silaha za moto kuwa ni la kisiasa. Wanaamini kuwa ni mchezo unaofanywa kisiasa ili kuondoa fikra za wananchi katika mambo yanayowakabili kama vile kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa, kujiandikisha katika daftari la wapiga kura na mengine.

Imefika wakati baadhi ya wananchi wanasema bila ya kuwa na uhakika wowote tena mbele ya watu wengine kuwa ni kazi ya Serikali. Yaani Serikali imetengeneza makusudi tukio la Tanga pasipo kuwahurumia wananchi wake.

Hii ni hatari ambayo si tu inaweza kuwachonganisha wananchi kuichukia Serikali yao bali inawezekana kuwa chachu ya kuanzishwa kwa vikundi vya uasi nchini. Lengo la wanaojaribu kuingiza hisia na chuki binafsi katika matukio mazito kama haya ya Tanga ni kujipalia makaa ya moto.

Wakati tukisherehekea maendeleo ya kisayansi na teknolojia ni lazima tuzijue athari zake hasi na chanya. Teknolojia imetusogeza karibu na kuwa mithili ya kijiji kimoja lakini inatupa nafasi ya kufungua fikra zetu ili zihariri yaliyosogezwa na maendeleo hayo.


Inatupa muda mwingine zaidi ya kutegemea wahariri wa magazeti,redio na televisheni kupitia na kuchuja kilicholetwa na maendeleo hayo yanayoonekana kukua kwa kasi. Mitandao ya kijamii si tu imeturahisishia kupata habari bali inatupa changamoto ya kuzithibitisha habari hizo.

Tunajua fika kuwa Jeshi la Polisi ndilo lenye kuweza kuthibitisha kuhusu mwenendo wa tukio hilo la Tanga ambalo bado linaendelea kusisitiza kuwa sio la kigaidi, hao wanaoandika kuwa ni Al Shabab wanatoa wapi na wana agenda gani? Na picha zisizohusiana na tukio zinatumika kwanini?

Taarifa zinazonasibisha Serikali au chama tawala kuwa nyuma ya mpango huu wa tukio la Tanga zimethibitishwa na nani? Kama ni kutumia mazowea tu inatosha kujikumbusha matukio ya uhalifu yaliyofanyika miaka ya nyuma kuwa nayo yalifanywa kwa baraka za Serikali au chama?

Wananchi tuamke kifikra sasa badala ya kutegemea uongo unaotungwa na baadhi ya watu huenda wasiolitakia mema taifa letu au kutokujua walitendalo. Kuna video mbalimbali zinasambazwa ili kuoanisha matukio ya kihalifu nchini, zisipuuzwe na kinyume chake bongo zipewe muda wa kuchunguza ukweli wake.


Tukio la Tanga linatosha kuwaamsha vijana ambao kwa asilimia kubwa ndio wahanga wa mchezo huu mchafu na watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii, kutokukurupuka na kuunga mkono harakati zisizoieleweka kichwa wala miguu.

0 maoni:

Chapisha Maoni

 
Top