Na Azard Mpango #UO 2
Bila shaka tumesikia
kwamba matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana (2014)
yametangazwa na kiwango cha ufaulu kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani
la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde kinaonekana kuongezeka kuliko mwaka juzi
(2013).
Dk. Msonde alisema kuwa
jumla ya watahiniwa 196,805 ambao ni
sawa na asilimia 68.33 (68.33%) ya watahiniwa wote walifaulu mtihani wa kidato
cha nne ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.08 (10.08%) ukilinganisha na mwaka
2013 ambapo wanafunzi 235,227 sawa na asilimia 58.25 (58.25%) ndio waliofaulu
mtihani.
Kumbukumbu zinaonesha
kuwa mwaka 2012 waliofaulu ni asilimia 43, mwaka 2011 asilimia 53.6, mwaka 2010
asilimia 50.4, mwaka 2009 asilimia 72.5, mwaka 2008 asilimia 83.6, mwaka 2007
asilimia 90.6, 2006 asilimia 89.12, na mwaka 2005 ni asilimia 89.3. Kifupi
sikumbuki kama kuna mwaka walifaulu asilimia mia moja kuanzia elimu ya msingi
mpaka sekondari.
Binafsi nawapongeza
waliofaulu mitihani ya kidato cha nne lakini nawakumbusha kuwa bado wanapaswa
kuomba Mungu zaidi kwa sababu kuna kigingi mbele yao cha kubahatika kuchaguliwa
kujiunga na kidato cha tano. Wapo
wanaochaguliwa na wapo pia wanaoachwa.
Kuchaguliwa kujiunga
kidato cha tano kwa wale waliofaulu mitihani ya kidato cha nne na kuchaguliwa
kujiunga na elimu ya juu kwa wale waliofaulu mitihani ya kidato cha sita ni
shughuli nyingine pevu. Si ajabu kuchaguliwa lisilo chaguo la mwanafunzi
(muombaji).
Hatua hii inamfananisha
mwanafunzi na mfungwa kwa jambo moja kwamba mfungwa hachagui gereza badala yake
ni bahati tu kupangiwa gereza alilokuwa akifikiri kupelekwa kama ilivyo
mwanafunzi anayewaza na pengine kuchagua shule au chuo, mchepuo au kozi na
hatimaye kutopelekwa huko apendapo.
Wapo wanafunzi wengi
ambao wamepangiwa wasichochagua na mfano mzuri ni ndugu yangu wa damu ambaye
alichagua michepuo ya Sayansi akachaguliwa kusoma kidato cha tano na sita
masomo ya Sanaa (Arts) na Chuo Kikuu alichagua kozi ya ‘Business
Administration’ badala yake akachaguliwa kujiunga kozi ya Elimu.
Hata kama kuna vigezo wanavyoviangalia
wachaguaji lakini ukweli unabaki kuwa tatizo kubwa wachaguaji hawana taarifa za
wanaowachagua. Hawajui hao wanaowachagua wanapendelea kozi au michepuo ipi na
kwanini?.
Kuchagua wanaotoka
darasa la saba kwenda sekondari kwa mfumo wetu wa elimu hakuhitaji kuwaumiza
wachaguaji kumfikiria wanayemchagua kwamba anapenda mchepuo gani kwa sababu
huko wanakwenda kuchanganya masomo yote labda kidato cha tatu ambapo pia ni juu ya walimu kujadiliana na wanafunzi kwa
kuangalia uwezo wa masomo ya darasani.
Kinyume na
anayechaguliwa kujiunga kidato cha tano,
kwanza anakwenda kusoma baadhi ya masomo kama ni Historia, Jiografia na Lugha
ya Kiingereza (HGL) ni hayo tu na anayeomba kuchaguliwa bila shaka
amejiaminisha kuwa amefanya vizuri masomo anayoomba kuchaguliwa na hivyohivyo
kwa waombaji wa elimu ya juu wanaomba kile wanachokimudu.
Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi Shukuru Kawambwa
Kitendo cha anayeomba
mfano masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM) halafu po akachaguliwa kusoma
masomo ya Uchumi, Jiografia na Hesabu (EGM) ni kumuharibia mapendekezo yake,
lakini kwa kuwa ni mfungwa hana namna zaidi ya kutumikia kifungo hicho.
Wale wa kidato cha sita
ambao mfano wanaomba kozi ya Sheria halafu wanachaguliwa kozi ya Elimu, bila
shaka kutakuwa na msuguano japo wa ndani ambapo kuna watakaosoma kwa shingo
upande, hali hii inaweza kupelekea kutokuwa na wataalamu waliopenda taaluma zao
tangu awali.
Kwa maana hii huenda
tusilalamikie utendaji mbovu wa wataalamu wetu kwa sababu inawezekana taaluma
walizosomea walilazimishwa na mfumo wa elimu au wachaguaji. Kuna kuna kazi
kubwa ya kuchagua wanafunzi waliofaulu kutokana na kile wanachokipenda ingawaje
wapo ambao wanatumikia kile walichoomba na kuchaguliwa. Wahitimu waombe Mungu
waangukie kwenye machaguo yao.
0 maoni:
Chapisha Maoni