Na Azard Mpango
Nimekumbuka maneno ya wahenga wetu waliposema kwamba
ukila na kipofu usimshike mkono. Nimeyakumbuka haya huku ikiwa imepita miaka
takribani saba tangu tushikwe mkono tukiwa kwenye sahani ya umasikini, lakini
ni siku chache tena hali hiyo imejirudia. Tumeshikwa tena.
Katikati ya mlo mwaka 2008 kipindi tukijua tupo
masikini peke yetu kwenye nyumba ya Tanzania, ghafla tukashikwa mkono na msomi
Andrew John Chenge tena alijisahau akasema kwa sauti kuwa zile dola milioni 40
za rada kwake si chochote ni ‘vijisenti’ tu. Aliwaambia waandishi wa habari
kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu J.K. Nyerere alipowasili akitoa nchini China.
Rada hiyo ilinunuliwa katika kipindi cha Rais
Benjamin Mkapa (sasa mstaafu) wakati Chenge aliyepata shahada yake ya pili ya
sheria (Master of Laws) katika chuo cha Harvard cha nchini Marekani, moja ya
chuo bora duniani alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Andrew Chenge
Waliomuona walimfuatilia mpaka wakagundua kuwa
alikuwa na akaunti nje ya nchi iliyokuwa na zaidi ya dola milioni moja. Kelele
za waliostuka zilipenya kiasi kwamba zilimpelekea Chenge kujiuzulu nafasi ya
Waziri wa Miundombinu aliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2006.
Wengine kwa upofu wetu tukadhaniwa hatujui na ndio
maana hata akateuliwa kuwa Waziri wa kwanza wa Afrika Mashariki (2006) na baadaye
Waziri wa Miundombinu (2006-2008). Kisa ni kule kukubali kumchagua mwaka 2005
kuliwakilisha jimbo la Bariadi Magharibi huku akijulikana fika kuwa amevamia
sahani wasioweza kuita dola milioni 40 ni vijisenti.
Katika hali ileile ya kujisahau kuwa wanakula na
nani, mwezi Februari 2015 mbunge wa Muleba Kusini Profesa Anna Kajumulo
Tibaijuka alisema kuwa alitoa mapema kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya
kununulia mboga. Alisema hayo kipindi akijitetea alipokuwa akihojiwa na
mwanasheria Getruda Cyriacus wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
kuhusu sakata la fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.
Anna Tibaijuka
Bado
wanaamini vipofu wanaokula nao hawana uwezo wa kuhisi hata wakiguswa na ndio
maana wanafanya watakavyo. Wanachojua watawakaribisha tu (kuwachagua) kwa kuwa
hawakuwaona wala kuwahisi kama nao waliokuwepo kwenye sinia ileile ya awali.
Roho nzuri ya vipofu (wananchi wanaowachagua) inawapa kiburi wenye macho
(viongozi).
Mengi yamepita ikiwemo falsafa ya ANGUKA (yaani
Ari,Nguvu na Kasi) na hayakuonekana na ndio maana panakuwepo na nguvu
inayoshawishi kauli za ajabu. Wananchi wanalia kila uchwao kutokana na kutoona
faida ya kukua kwa pato la taifa, kushindikana kuwakabili kikweli maadui wa
Tanzania aliowataja baba wa taifa na bado kimya kinatawala.
Ifike wakati viongozi wetu wajue kwamba wanawaongoza
watu wengi wasiokuwa na uwezo sio tu wa kuziona dola milioni 40 ni vijisenti au
kutumia milioni 10 kwa ajili ya mboga bali hiyo milo mitatu kwa siku ni shida,
hivyo wachunge wanachokisema hata kama ni kweli. Viongozi wawe waogopa wa kutoa
maneno pasipo kuyapima mara mbili kwa sababu yanaweza kuinua hasira za wananchi
wanaowatarajia wawapigie kura katika chaguzi mbalimbali.
N.B: sikutumia neno vipofu kwa ajili ya kuonesha
dharau ya kundi hili bali nimelazimika kutumia kutokana na methali niliyoanza
nayo, samahani kwa yeyote aliyekwazika na hilo.
0 maoni:
Chapisha Maoni