Na Azard Mpango
Mwandishi wa vitabu ambaye pia ni Mhadhiri mzaliwa
wa Missouri katika jimbo la Florida nchini Marekani, Samuel Langhome Clemense
aliyekuwa akipendelea kuitwa Mark Twain alipata kusema kwamba hofu ya kifo
hutokana na hofu ya kuishi.
Mark Twain mwandishi wa kitabu kitwacho “Adventures
of Hucklebery Finn (cha mwaka 1885) ” aliyezaliwa Novemba 30, 1835 na kufa
Aprili 21, 1910 huko Redding, Connecticut nchini Marekani katika nukuu yake
alisisitiza kwamba mtu aliyehai hujiandaa kwa kifo kitakachomfika muda wowote.
Maneno haya yenye nguvu katika bongo za wenye
kufikiri yalinigusa pale nilipopata taarifa ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa
jimbo la Mbinga Magharibi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kapteni (mstaafu)
John Damiano Komba ambaye alikufa akiwa njiani wakati akipelekwa hospitali ya
TMJ ya jijini Dr-es-Salaam.
Taarifa za awali kuhusu kifo cha mbunge huyo ambaye
pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa kikundi cha sanaa cha Tanzania One Theatre (TOT)
na mwimbaji maarufu nchini nilizipata kupitia mitandao ya kijamii hasa ‘Facebook’
na ‘WhatsApp’ ingawaje zilionesha vyanzo vya taarifa hizo ikiwemo Redio Uhuru
inayomilikiwa na CCM.
Sikushtushwa na taarifa za kifo cha Kapteni Komba
kwa kuwa niliamini kwamba kwa mwanadamu kufa si kiroja kama anavyojihakikishia
mcharaza gitaa Johnny Allen Hendrix (Jimi Hendrix) aliyezaliwa Novemba 27, 1942
pale Seattle, Washington nchini Marekani kuwa yeye ni miongoni mwa watakaokufa
pale muda utakapotimu. Hata Kapteni Komba ni miongoni mwao!
Nilishangazwa na namna wapokeaji walivyotoa maono
(comments) yao ambayo mengi niliyoyaona yalikosa huruma na simanzi ya kiutu na
kinyume chake yalijaa kebehi, chuki zilizojengwa kisiasa na laana kwa Kapteni
Komba. Yalikuwapo maneno makali kiasi cha mengine kumhukumu kabisa hata kabla
ya kuwekwa kwenye makazi mapya (kaburini).
Hata salamu za kumtakia mapumziko mema (Rest In
Peace) za wengi wao zilikuwa na shida kwa sababu ziliandikwa kimazowea na sio
kuagizwa na nyoyo za huruma zinazomsukuma mwanadamu kuguswa na kifo cha kiumbe
mwenzake anayemithilika naye. Hesabu za haraka zilitoa majibu kwamba ‘R.I.P’
nyingi kama sio zote zilikuwa za wana-CCM na waliozowea ama kujisikia uvivu
kutoa ‘comments’ zao.
Lengo si kumsafisha Kapteni Komba aliyeishi zaidi ya
miaka 50 ulimwenguni tena kwenye gurudumu lenye mikimiki la siasa kama za
Tanzania bali kukitazama kifo chake kama shule kwa waliobaki. Natambua fika
kwamba mahali alimopita marehemu enzi ya uhai wake kuna mambo mabaya au pengine
ya kuudhi aliyatenda ama kuyasema lakini kurasa zake zimefungwa na hakuna wa
mwanadamu wa kuzisahihisha tena halafu akamrejeshea.
Hayo yanabaki kuwa ni majeraha kwa walioguswa na
zaidi katika maisha ya mwanadamu aliyeishi umri kama wa Kapteni Komba na hata
pengine wa chini yake hawezi kusalimika na madonda ya lawama kwa sababu si kila
alifanyalo maishani mwake wanajamii watalipokea kwa mikono miwili na ukarimu.
Hivyo mwanasiasa huyu ameondoka na makovu yake kama
vile anavyojiapiza mwandishi wa riwaya na nyimbo, Charles Michael Palahniuk
(Chuck Palahniuk) aliyezaliwa eneo liitwalo Pasco pale Washington pindi
aliposema kuwa hawezi kufa bila ya makovu. Na vivyo hivyo ndivyo alivyokufa
Mjumbe wa Kamati Kuu (NEC) ya CCM.
Marehemu John Komba
Funzo kubwa kutokana na vifo vya wanadamu kikiwemo cha Kapteni Komba ni
kujisahihisha na kujitathmini badala ya kuwalaumu waliokufa. Uhai si wasaa wa
kuanza kuhesabu mema na maovu ya marehemu bali ni nafasi adhimu ya kupanga
namna ya kuiacha dunia. Si nafasi ya ‘kupost’, ‘kuchat’ au kupoteza muda kwa
waliohai bali ni kipindi cha maandalizi ya kifo, hivyo kunahitajika kujipanga
kwa sababu utaacha majeraha.
Kapteni Komba aliyezaliwa Machi 18, 1954 na kufa
jioni ya Februari 18, 2015 alipata kusema kuwa mwanadamu anapaswa kujua kuwa
kufa kupo ingawaje si vyema kukifikiria lakini mchekeshaji na mwandishi, Allan
Stewart (Woody Allen) aliyezaliwa Disemba 1, 1935 alipata kusema kuwa haogopi
kufa bali hataki kuwepo pale (kifo) kinapotokea.
Tuliokuwa hai sasa ni wafu wa baadaye, tujitahidi kutumia
vyema fursa ya uhai wetu kwa sababu hata Kapteni Komba hakujua kama ni 2015
ndio kifo chake huenda angejisahihisha na kuomba msamaha kwa aliyowakosea. Kifo
chake ni hofu kwetu.
0 maoni:
Chapisha Maoni