Na Azard Mpango
Wataalamu ni watu muhimu katika jamii. Nchi yoyote
duniani inahitaji kuwa na wataalamu wa fani mbalimbali ili kuweza kupata
maendeleo kuanzia ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyotolewa na Taasisi ya
Uchung uzi wa Kiswahili (TUKI) toleo la tatu imetoa maana ya neno mtaalamu
ambalo wingi wake ni wataalamu kuwa ni mtu mwenye elimu, ustadi au ujuzi wa
fani au jambo Fulani maalum. Na hata Tanzania watu hao wapo.
Kazi ya wataalamu ni kutumikia kile walichosomea au
walichokuwa na ujuzi nacho. Mfano mtaalamu wa masuala ya uchumi aoneshe umwamba
wake katika uchumi, wa siasa na siasa na elimu naye kwenye elimu. Kifupi ni
kwamba kila mtaalamu anapaswa atumikie
utaalamu wake.
Kwa maana hiyo tulitarajia taifa letu ambalo lina
wataalamu wengi mno wa fani mbalimbali lingepiga hatua. Wataalamu wetu
wangesaidia kwa kiwango kikubwa kama sio chote nchi yetu kutononoka.
Lakini kama vile siasa ya nchi yetu imewakataza
wataalamu kutumikia utaalamu wao na badala yake inawafunga kamba na kuwaburuza
waingie kwenye kwenye jengo la maamuzi ya kisiasa mahali ambapo utaalamu sio
kigezo kikubwa cha kupewa kiti cha heshima.
Nao pasipo kujali hilo wameamua kutundika vyeti vyao
na kuacha kutumikia kwa wasaa mpana utaalamu wao na kuamua kukimbilia katika
siasa.
Wataalamu hawajifungii ndani au kuzuunguka huku na
kule kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali bali wanachofikiria ni namna ya
kuwa wabunge, madiwani na pengine Rais, basi.
Siasa imewateka wataalamu wetu wengi ijapokuwa sio
wote kama vile wa afya, sheria, elimu, uchumi na wengine wa fani tofauti. Wengi
wao hawatumikii tena utaalamu wao bali wanatumikia siasa ambayo kuwashushia
heshima zao si kazi ngumu kwasababu haijali utaalamu.
Huenda ni kwa sababu mfumo wa siasa uliopo
unaonekana kusita kumtazama mtaalamu kinyume chake unamtaza zaidi mwanasiasa.
Marupurupu, mishahara minono na pengina hata posho nzuri anazopata mtaalamu ni
tofauti na mwanasiasa ambaye huenda hana hata utaalamu wa siasa anayoitumikia.
Kivutio kikubwa cha maslahi kilichopo kwenye siasa
kimekuwa ni chambo wa kuwapata wataalamu wetu kukimbilia huko pasipokujali
kudhalilika. Heshima na hadhi zao zinagaragazwa hadharani kiasi cha kuwatia
aibu, lakini wenyewe hawajali kitu.
Wataalamu wameamua kuipigia magoti siasa badala ya
kutumikia utaalamu wao ambao ungeweza kuibadili siasa yenyewe. Wataalamu wetu
ambao kimsingi ni kundi muhimu katika jamii wametumbukia kwenye dimbwi lenye
tope linalotoa harufu mbaya kiasi cha kuwatukanisha mbele ya jamii.
Utaalamu wao sio heshima tena kwa jamii na ndio
maana mpaka vinywa vya wasioweza kuwafikia vimethubutu kuwaita majina
yasiyopendeza na yanayoonesha kutojali utaalamu wao. Aibu wanayopata inachafua
na hata kutia walakini utaalamu wao. ‘Eeee! Mola waopoe wataalamu wetu.’
0 maoni:
Chapisha Maoni