Na Leonard Kadago #UO 3
Katika maisha ya kawaida kuna binadamu ambao tangu wamekufa
hakuna aliyezaliwa kuziba mapengo yao. Hali hiyo inatokana na uwezo mkubwa wa
kufanya ambo mbalimbali pamoja na busara
walizojaliwa na Mungu.
Miongoni mwa watu hao ni mwanamapinduzi Thomas Isidore
Sankara aliyezaliwa Disemba 21, 1949 maeneo ya Yako, French Western African
(Burkina Faso ya sasa) aliyeuawa Oktoba 15, 1987 Orgadou, Burkina Faso.
Sankara mwanajeshi aliyefikia cheo cha Kapteni aliyepata
kuwa Rais wa Burkina Faso kati ya 1983 na 1987 aliwagusa wengi kiasi kwamba
wananchi wa Burkina Faso wamefikia kukiri kuwa hakuna Rais aliyefanana naye au
kumkaribia kutokana na uzalendo pamoja na uaminifu aliokuwa nao kwenye
rasilimali za taifa hilo lililopo Magharibi mwa Afrika.
Mifano ya watu kama Sankara ipo mingi mno katika maisha yetu
ya kila siku kuanzia kwenye ngazi ya familia, kata, wilaya, mkoa na taifa kwa
ujumla wake. Kuna watu wengi hasa viongozi ambao wamefanya mambo mengi mazuri
ambayo hakuna binadamu aliyewakaribia.
Watu hao si tu wapo kwenye masuala ya siasa peke yake bali mpaka kwenye michezo. Wapo hadi kwenye soka
letu la nyumbani na mpaka kwenye Ligi
Kuu yetu ya Vodacom. Wapo mpaka kwenye klabu zetu za bongo ikiwemo na kikosi cha Simba maaarufu
kama Wekundu wa Msimbazi.
Marehemu Patric Mafisango
Kumbukumbu chungu kwa Wana Msimbazi ni ile iliyotokea Mei
17, 2012 ambapo walimpoteza kiungo mkabaji aliyekuwa na uwezo wa hali ya juu wa
kutumia guu lake la kushoto kila anapokuwepo uwanjani. Huyo ni Patrick Mutesa
Mafisango aliyezaliwa Machi 9, 1980 pale Kinshasa, Zaire aliyekufa njiani
wakati akikimbizwa hospitali baada ya kupata ajali ya gari jijini Dar es
Salaam.
Hakuna shabiki wa
Simba na pengine hata wa klabu nyingine ambaye atalisahau jina la Mafisango
aliyekuwa na asili ya Kongo ambaye alichukua uraia wa Rwanda. Jamaa alikuwa
anaujua na alifanya kazi yake kwa ustadi wa hali ya juu na ndio maana aligeuka
na kuwa kipenzi cha mashabiki wa soka na hasa wa klabu ya Simba.
Kifo cha Mafisango kimeacha pengo kubwa kwa wana Msimbazi na
wapenda soka nchini. Kimewaacha wengi midomo wazi lakini furaha kwa klabu ya
Simba imeanza kurejea baada ya kumpata kiungo ambaye uwezo wake unafanana na
ule wa Mafisango. Kiungo huyo anatumia mguu kama wa Mafisango.
Kwa wale waliobahatika kutazama au kufuatilia mechi za hivi
karibuni ilizocheza klabu ya Simba na Coastal Union pamoja na ile
iliyowakutanisha na Polisi Morogoro bila shaka watakuwa wamemuona mchezaji
aliyevaa jezi namba 24 mgongoni.
Ni Abdi Banda ambaye
alisajiliwa kama beki akitokea klabu ya Coastal Union lakini ujio wa kocha
kutoka Serbia Goran Kopunovic umekuwa kama neema inayowakumbusha mbali wana
Msimbazi kwa sababu kocha huyo amembadili namba kutoka kucheza nafasi ya beki
mpaka kiungo mkabaji.
![]() |
Kiungo wa Simba Abdi Banda |
Kila mpenda soka anapata furaha moyoni kumtazama kiungo huyu
kutokana na ukweli kuwa huwa anafanya kazi yake kwa kujituma na kila pasi
anayotoa inafika palipostahili na ni mara chache kupoteza mpira. Banda ana umbo
la kimpira na hasa urefu wake unamfanya kugeuka burudani wa kila anapogusa mpira.
Iwapo mchezaji huyu wa
klabu ya Simba atajifunza na kutolewa sifa
bila shaka ataisaidia klabu yake pamoja na timu ya taifa kutokana na
ukweli kwamba umri wake unaruhusu.
Shughuli yake awapo uwanjani inawafunika viungo wengi wa nyumbani.
Yote tisa, kumi ni kile kiwango alichokionesha katika
pambano la Watani wa Jadi (Simba na Yanga)lililofanyika Machi 8, mwaka huu kwenye uwanja wa taifa
lililoishia kwa Simba kushinda goli moja lililowekwa kimiani na Emanuel Okwi.
Banda alifunika safu ya kiungo ya watani wao iliyokuwa
ikiongozwa na Haruna Niyonzima. Alikaba kwa nguvu na alitandaza pasi zenye
macho muda wote wa mchezo huo. Uwepo wa Banda na kiwango anachokionesha akiwa
na uzi wa Simba kinakumbusha uwepo wa Mafisango mwingine.
Miaka ya hivi karibuni
klabu ya Simba imezalisha wachezaji wengi vijana kama vile Jonas Mkude, Saidi Ndemla, Abdallah
Seseme, Ramadhani Singano, Ibrahim
Ajibu, Haruna Chanongo pamoja na nahodha wa timu hiyo Hasani Isihaka
lakini ujio wa kijana Banda anayetumia mguu wa shoto kama Mafisango ni faraja kwa wana Simba na wapenda soka
safi. ‘Bravo Abdi Banda’ lakini usilewe sifa.
0 maoni:
Chapisha Maoni