Na Azard Mpango
Kwani kuna ambaye hajui kama bajeti ya nchi yetu inapitishwa
na wanasiasa? Kuna asiyetambua kwamba kilimo kinachoitwa uti wa mgongo wa taifa
hili nacho kinasimamiwa zaidi na wanasiasa? Hivi kweli kabisa huenda akatokea
mtu aseme kuwa hajui kama elimu yetu ipo chini ya uangalizi na usimamizi wa
wanasiasa?
Jamani!Hata ulinzi na usalama wetu nao hatujui kama upo
chini ya himaya ya mwanasiasa? Hapana, huyu ni lazima nimtaje. Yeye ndiye amiri
jeshi mkuu anayepigiwa saluti na wanausalama wote. Ndio mpaka afya zetu
wanaopitisha bajeti yake ni wanasiasa tu na sio wengine. Hakuna kinachofanyika
chini ya jua la nchi yetu lisiwe na mkono wa wanasiasa kwa sababu bajeti nzima
inapitishwa na haohao.
Kifupi tunaweza kusema kwamba maisha yetu yote yapo chini ya
mwamvuli wa siasa na kwa maana hiyo tusiifanyie mzaha. Ndio, tusicheze kabisa
na siasa kwa sababu tutakuwa tunachezea maisha yetu wenyewe. Kwani si mnajua
kama katiba ya nchi ambayo ndio sheria mama nayo miongoni mwa walioitunga na
kuipitisha ni wanasiasa?
Hata katiba inayopendekezwa, wanasiasa walikwuwepo nahata jengo
lililotumika ni lilelile linalotumiwa na wanasiasa kila uchao na uchwao. Si utani
jamani siasa ndio yenye nguvu na nafasi kubwa kuliko chochote Tanzania na ndio
maana hata wanataaluma bobezi nao hawashikiki kwenye siasa. Huko kuna ‘mshiko’
wa maana hata kama pakiwa kuna fujo na vurugu.
Lakini hata hivyo ukiachana na nafasi iliyokuwa nayo siasa
hapa nchini, bado hatuwezi kuacha kusema kuwa ni mchezo mchafu. Mara ngapi
mfano kule bungeni kumetokea vurugu? Nani hakuwahi kushuhudia washa zima
maikrofoni inayofanywa na waheshimiwa wanasiasa (wabunge) ambao ndio
tumewaamini wakatuwakilishe? Ni kweli tumewatuma wakaropoke au kupiga kelele zisizokuwa
na natija kwetu?
Tumewatuma wakatetee maslahi ya vyama vyao na matumbo yao?
Tukubali tu kwamba siasa ni mchezo mchafu unaowachafua wengi,
wake kwa waume na vijana kwa wazee. Imechafua upande wa vyama vya upinzani na
chama tawala. Inawachafua wasomi wetu na wanataaluma waliofurika huko.
Mtangazaji wa masuala ya siasa John Calvin Thomas (Cal
Thomas) aliyezaliwa Disemba 2, 1942 katika jimbo la Washington D.C nchini
Marekani,anasema kuwa sababu mojawapo ya watu kuichukia siasa ni kwamba ukweli
ni mara chache kuwa lengo la mwanasiasa. Hii ina maana kuwa wanasiasa wengi
kama sio wote hawaupi ukweli nafasi yake hasa kwenye malengo yao ya kisiasa
mbele ya wananchi.
Wanajiona wamepewa nafasi ya kuchezea bongo za wananchi.
Wanaona hakuna tatizo kuahidi ingawa wanatambua fika hawataweza kutekeleza. Wanajizatiti
kutembea juu ya mabega ya walalahoi wanaominywa kodi zao kwa ajili ya kulipwa
mishahara na posho pasipokujua kuwa ipo siku nao wanastuka na kuwashusha kwa
nguvu mwilini mwao.
Bado siasa itaendelea kuwa mchezo mchafu mpaka pale
wanasiasa watakapoamua kuusafisha kwa kutumia ukweli kwa asilimia mia moja kama
moja ya lengo lao. Utakuwa mchezo msafi pale wanasiasa watakaposhuka mabegani mwa
wananchi na kuwaambia kuwa waliwanyonya kwa muda mrefu kwa kutumia mrija wa
siasa, waliwadanganya mengi ili wapate ushindi na walipambana kwa ajili ya
vyama vyao na wengine maslahi yao binafsi kabla ya kuwatumikia wananchi
waliowatuma.
0 maoni:
Chapisha Maoni
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.