Na Azard Mpango

Muigizaji ambaye pia ni mchekeshaji, Roseanne Charrie Barr aliyezaliwa Novemba 3, 1952 huko Salt Lake City nchini Marekani alipata kutoa somo kwa wanawake wenzake kwamba jambo moja wanalotakiwa kujifunza ni kuwa hakuna yeyote atakayewapa nguvu (power), hivyo wanatakiwa wachukue.

Bila shaka aliyasema hayo kutokana na historia ya kuteseka na kutengwa kwa wanawake ulimwenguni. Atakuwa ameyakumbuka machungu waliyopata wanawake wenzao na pengine kuna maeneo mpaka sasa bado wanaendelea kuyapata ingawaje ni tofauti na zama zilizopita.

Amekumbuka namna mwanamke alivyochukuliwa kuwa ni chombo cha starehe pekee na sio vinginevyo. Mwanamke hakuonekana ni kiumbe bora mbele ya mfumo kandamizi unaohisiwa kwamba mpaka leo bado haujafutika na umeendelea kukita mizizi yake tena mpaka katika fikra za binadamu wa karne ya sayansi na teknolojia.

Kwamba bado mawazo mgando ya kumdhania mwanamke kuwa ni mshindwa yangalipo ijapokuwa sura ya mwanamke mwenyewe inaonekana karibu kila mahali. Si katika majeshi, uongozi mbalimbali, michezo, viwandani, biashara na maeneo mengine mengi tu mwanamke naye yupo. Leo mpaka kumimina zege nao wanajichanganya.

Kule kulikoitwa kupigania haki za wanawake kunaonekana kupatikana kwa matunda yake ingawaje si kwa kiwango kikubwa. Vita ya kuwatetea wanawake haipaswi kukoma kwa sababu ya kuonekana kwamba wameanza kupumua kwa kushirikishwa karibu katika kila mahali kuanzia ofisini mpaka nyumbani.

Sauti kali ya utetezi isishuke na badala yake ipazwe ili iende zaidi ya hapa ilipo sasa. Anayenadi asiogope kukauka koo kwa sababu birika lililojaa maji yenye baraka linakuja. Kila nchi kwa nafasi yake isichoke kuwapa nguvu wanawake ikiwa ni pamoja na kutunga kanuni na sheria zitakazotilia uzito suala hilo na sio kuwabeba.

Ni lazima ieleweke kuwa wanawake hawapaswi kupewa upendeleo wa aina yoyote bali wapewe nguvu na ndio maana hata mwanamama Roseanne amewakumbusha hilo. Kumpa mwanamke upendeleo si kumuinua wala kumtoa kwenye mfumo dume unaopigwa vita bali ni kumlemaza na kumuhakikishia kwamba ni kiumbe dhaifu anayengoja kubebwa kwa kila kitu.

Lakini kama vile wanawake wenyewe nao hawalioni hili au wanaogopa kukataa. Ule unyonge wao uliokuwepo tangu zama na zama unaendelea kwa aina tofauti kidogo siku hizi. Enzi zile walinyongeshwa pasipo kutarajia kinyume na enzi hizi ambazo kwa mikono yao miwili wanapokea aina zote za unyonge tena kwa furaha.

Ukimya wa wanawake wengi wa Tanzania dhidi ya kaulimbiu zenye ukakasi kwao ni ishara kwamba wameanza kusahau kama wenzao walipitia kwenye njia zenye miiba kabla ya kufika hapa ilipo leo. Wenzao waliosimama kidete kutetea haki za wanawake hawakutaka upendeleo wa aina yoyote zaidi ya nguvu.

 Wanaambiwa eti wakiwezeshwa wanaweza! Wao wanarukaruka kwa mapambio. Kwanini wasihoji kuwezeshwa huko? Mbona wanasahau kwamba waliambiwa wachukue na sio kusubiri kuwezeshwa kama wanavyofanya siku hizi?

Wanasubiri kupewa ubunge wa viti maalum. Wanasubiri alama za chini za wastani wa kufauluhuko mashuleni na wanasubiri huruma na upendeleo karibu kila mahali. Huku ni kurudishwa nyuma tena wakati wapambanaji walishaanzisha na kilchobaki ni muendelezo wa kuchukua na sio kupendelewa.

Wanawake wa Tanzania wanaendelea kutengeneza unyonge usiomithilika iwapo wataendelea kupokea nafasi za upendeleo badala ya kuchukua nafasi zao. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 si inasisitiza kuwa kila binadanu huzaliwa akiwa huru na sawa, sasa ni kwanini wanawake washindwe mpaka wawezeshwe?

Leo tunaelekea katika uchaguzi mkuu lakini kutokana na kujisahau kama wanawake ni sehemu ya binadamu huru na sawa kama walivyokuwa wanaume bila shaka hawataonekana katika foleni ya kuchukua fomu za kuomba kugombea Urais. Sio hawawezi bali wameshajishusha zaidi ya walivyoshushwa wanawake wa zama zilizopita.


Mpaka sasa historia ya Tanzania imemuandika Anna Claudia Senkoro akiwa mwanamama pekee aliyethubutu kutaka kuchukua nguvu (power) mbele ya wanaume tisa waliokuwa  wakigombea nafasi ya Urais. Inawezekana kabisa waliompinga na pengine kumbeza asilimia kubwa kama sio yote ni wanawake wenzake. Wenyewe hawapendani na hawaaminiani.


 Kama wanawake nchini hawajaamua kuachana na woga unaowapelekea kutojiamini wataendeleza kuusimika mfumo kandamizi dhidi yao kutokana na ukweli kuwa wenyewe wanaufurahia nakuukumbatia. Ifike wakati wanawake waachwe wasimame kwa nguvu zao wenyewe na sio kupendelewa.
26 Mar 2015

0 maoni:

Chapisha Maoni

:) :)) ;(( :-) =)) ;( ;-( :d :-d @-) :p :o :>) (o) [-( :-? (p) :-s (m) 8-) :-t :-b b-( :-# =p~ $-) (b) (f) x-) (k) (h) (c) cheer
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.

 
Top