Na Azard Mpango
Wachezaji wa Tanzania mpo? Mmemuona au kumsikia Mrisho
Khalfani Ngasa anayechezea klabu kongwe ya Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935 yenye
makao makuu yake Jangwani? Mmemuelewa alichosema?
Ngasa ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania
aliyezaliwa April 12, 1989 jijini Dar-es-Salaam, anayecheza nafasi ya
ushambuliaji na kupendelea kuvaa jezi namba 17 alionekana kujilaumu waziwazi
kwa kukataa kwake kujiunga na klabu ya Al-Merikh ya nchini Sudan kisa mapenzi
yake kwa klabu ya Yanga. Ameeleweka?
Mshambuliaji huyo ambaye ni mtoto wa mchezaji wa zamani wa
klabu hiyo ya Yanga, alikataa mpango wa timu yake ya Azam iliyomsajili kwa
gharama kubwa na timu ya Simba aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo katika msimu wa
2012/2013 zilizotaka kumuuza Al-Mereikh.
"Nimekuwa nikikataa dili nyingi ninazopata kwa sababu
ya mapenzi yangu ya Yanga," alisema Ngasa aliyewahi kuitumikia klabu ya Kagera
Sugar msimu wa 2005/2006, Yanga 2006/2010 na baadaye Azam msimu wa 2010/2013
ambapo klabu ya Azam ilimpeleka klabu ya Simba kwa mkopo na kuitumikia msimu wa
2012/2013.
Ngasa aliyewahi kuwa mfungaji bora mwaka 2009 katika
mashindano ya kombe la Kagame wakati akiitumikia timu ya taifa lake, kama vile
ameipiga teke bahati katika soka ingawaje kwa umri wake lolote linaweza
kutokea. Lakini kwa sasa Ngasa anajuta kubaki Yanga kisa anaipenda.
![]() |
Mrisho Ngasa akitumikia Taifa Stars |
"Leo ninajuta, nakumbuka nafasi hiyo niliyoipata
kupitia Simba na Azam ndio ilikuwa bahati yangu ya kutoka kisoka,"
anasisitiza winga huyo aliyewahi kufanya majaribio mwaka 2009 katika klabu ya
West Ham inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza.
Pia baadaye mwaka 2011, Ngasa alibahatika kufanya majaribio
mengine nchini Marekani katika klabu ya Seattle Sounders iliyowahi kucheza
mechi ya kirafiki na klabu ya Manchester United ya Uingereza na Ngasa alicheza
mechi hiyo akitokea benchi.
Leo winga huyo anasikitika ingawa anakiri hana wa kumlaumu
zaidi ya nafsi yake. Wachezaji wanaojali zaidi ya mapenzi ya klabu zao na
hatimaye kubaki hata ikitokea bahati ya 'mtende ya kuota jangwani', hebu
wajifunze kwa mwenzao Ngasa.
Usijadili ubora wa Al-Mereikh dhidi ya Yanga kwa sasa kutokana na ukweli kuwa mchezaji
mwenyewe ameona kwenda huko kungemsaidia kutoka zaidi kisoka kuliko kubaki
kwenye klabu anayosisitiza kuipenda.
Tujadili idadi ya wachezaji wanaokubali kusota benchi katika
klabu zao kisa wanazipenda na kukataa kwenda klabu nyingine. Tujadili madhara
kwa wachezaji hao ikiwemokuporomoka kwa viwango vyao na hasara inayoweza
kuigharimu pengine mpaka timu ya taifa. Tujiulize kwamba wachezaji hawa
wanajielewa kweli?
Ni lazima kuwa wawazi kwamba mchezaji kupenda timu yoyote
sio mwiko wala dhambi na ndio maana tunamuona nahodha wa klabu ya Liverpool,
Seven Gerrard aliyezaliwa Mei 30, 1980 pale Whiston, Merseyside nchini
Uingereza namna anavyoipenda klabu yake iliyomlea tanghu mwaka 1987 na bado
anaitumikia.
Ni vigumu kumlinganisha Ngasa na Gerrard kwenye upande wa
mapenzi ya klabu zao kutokana na jambo moja tu kwamba Gerrard hakupata kujuta
kubaki katika klabu anayoipenda ya pale Anfield kama Ngasa alivyoijutia klabu
anayoipenda ya pale Jangwani. Hapa kuna masafa!
Winga machachari wa Yanga, Mrisho Ngasa, akimtoka beki wa Ruvu Shooting, Stepano Mwasika, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom. |
Sasa ni muda wa wachezaji wetu wa 'kibongo' kufungua macho
ya kufikiri ili waweze kumuona Wayne Mark Rooney aliyezaliwa Oktoba 24, 1985
pale Croxteth, Liverpool nchini Uingereza. Rooney alilelewa katika klabu ya
Everton tangu mwaka 1996 na anauthibitishia ulimwengu kuwa hakuna klabu
anayoipenda na kuishabikia zaidi ya Everton.
Nani hajui kama Rooney anaitumikia Manchester United? Nani
atashindwa kujibu swali kwamba kwanini Rooney ameiacha klabu anayoipenda
inayotumia uwanja wa Goodison Park na kuhamia kwa 'Mashetani Wekundu'
wanaotumia uwanja wa pale Old Trafford? Na lini tumemsikia Rooney ameujutia
uamuzi.
Ngasa ametoa somo la bure kwa wachezaji wetu karibu wote
hapa nchini hivyo wajifunze. Wakumbuke kwamba kama mapenzi pekee ya timu
yanatosha kumbakiza mchezaji hata kama atasota benchi basi angebaki Raul
Gonzalez Blanco pale Santiago Bernabeu.
Raul aliyezaliwa Juni 27, 1977 pale San Cristobal de Los
Angeles nchini Hispania, aliipenda klabu ya Real Madrid (Los Blancos), timu
iliyomlea tangu mwaka 1992 na mpaka akapewa heshima kuwa 'alama ya timu,'
lakini baada ya miaka 16 ndani ya Real Madri alitimkia Shalke 04 ya nchini
Ujerumani. Wachezaji wajifunze!
0 maoni:
Chapisha Maoni
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.